Mganga Mkuu Singida Aamua Kuacha Kazi Baada ya RC Kumsweka Rumande, Kisa Kipindupindu
SINGIDA:
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Singida Vijijini, Dk. Erick Bakuza ameandika
barua ya kuacha kazi ikiwa ni siku chache tangu alipopewa adhabu ya
kuwekwa mahabusu na Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Rehema Nchimbi.
Dk. Nchimbi alitoa amri ya kukamatwa
kwa daktari huyo kutokana na kuzuka ugonjwa wa kipindupindu ambao
ulisababisha vifo vya watu wawili mwishoni mwa mwaka jana.
Taarifa za kuacha kazi kwa Dk. Bakuza zimethibitishwa na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Rashid Mandoa.
“Ni kweli amewasilisha barua ya
kuacha kazi lakini ninavyojua mimi si kweli kwamba ameacha kazi kutokana
na adhabu aliyopewa na Mkuu wa Mkoa ya kuwekwa ndani.
“Kwanza ujue hakuwekwa ndani, na
ameamua kuacha kazi kwa sababu amepata sehemu nyingine ambayo anaona ina
maslahi anayohitaji yeye,” alisema.
Juhudi za kumpata Dk. Bakuza kuzungumzia hatua yake hiyo hazikuzaa matunda.
Kauli ya Mkuu wa Mkoa
Wakati Mkurugenzi huyo akisema kwamba
Dk. Bakuza hakuwekwa ndani, Mkuu wa Mkoa huyo, Dk. Nchimbi alithibitisha
kwamba aliwekwa ndani kwa saa tatu.
“Mimi nilitoa amri ya kukamatwa
Daktari huyu na aliwekwa chini ya ulinzi kwa saa tatu.Nilimuweka ndani
kwa sababu ya mazingira ambayo niliyakuta nilipokuja kuanza kuitumikia
nafasi niliyoteuliwa ya ukuu wa mkoa, na nitatetea uamuzi wangu huo.
“Niliamuru akamatwe kwa sababu ya
mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu, kesi ya kwanza ya kuwapo kwa mgonjwa
wa kipindupindu iliripotiwa Novemba 26, mwaka jana.
“Utaratibu unajulikana wazi kwamba
ikifika kesi tano DMO (Mganga Mkuu wa Wilaya) anatakiwa atoe taarifa kwa
MRO (Mganga Mkuu wa Mkoa).
“Desemba 4 hakutoa taarifa, ilipofika Desemba 16 vikatokea vifo viwili hakutoa taarifa hadi Desemba 18 ndipo akatangaza.
“Nikaona hakuwa makini katika kazi
yake kwa sababu alipaswa kutangaza mapema ili tuchukue hatua za
kudhibiti ugonjwa huo na naamini hata hivyo vifo visingetokea,” alisema.
Dk. Nchimbi alisema suala la kipindupindu halipaswi kuchukuliwa kisiasa na kwamba lenyewe lipo kitaalamu zaidi.
“Kuna taratibu ambazo hufuatwa
lazima tupate evidence ya kutosha, watu wachukuliwe vipimo, yeye
alinyamaza kimya. Wataalamu walipokwenda kuchunguza wakagundua kuna
kipindupindu kwenye wilaya yake,” alisema.
Aliongeza: “Kwa hali hiyo niliona hakuwa makini katika kazi yake, hivyo nilitaka kumshtua tu awe makini, hakuwa makini.
“Katika hali ya kawaida angesema
mapema tungechukua hatua mapema, tungetibu maji, tungesafisha visima na
hata vifo visingetokea,” alisema.
Comments
Post a Comment