Simba na Yanga zioneshe ukongwe wao uwanjani
PAMBANO la watani wa jadi katika soka la Tanzania la Simba na Yanga linafanyika leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Hilo ni pambano la marudiano baada ya lile la raundi ya kwanza kumalizika kwa sare ya kufungana bao 1-1 na baadhi ya mashabiki wa Simba kuleta vurugu kwa kuvunja viti vya uwanjani humo pamoja na vitu vingine.
Uwanja huo ni wakisasa na wathamani kubwa na umejengwa kwa kodi za wananchi, hivyo kuharibu miundo mbinu yake ni kutowatendea haki Watanzania, ambao wengi wao ni wale wa kipato cha chini.
Ni matarajio yetu kuwa, baada ya maandalizi ya muda mrefu ya timu hizo kwa ajili ya pambano hilo, bila shaka mchezo utakuwa mzuri utakaowafanya mashabiki kufaidi fedha zao walizotoa kwa ajili ya viingilio.
Na uzuri wa mchezo wa soka sio timu kucheza vizuri, bali pia waamuzi kuchezesha kwa haki kwa kutumia sheria 17 za soka, mashabiki kuwa watulivu na mambo mengine kibao.
Simba na Yanga ni timu kongwe kabisa hapa nchini, hivyo ni matarajio yetu kuwa, timu hizo zitaonesha ukomavu huo kwa kucheza soka litakalotoa burudani na kuwafurahisha wapenzi wa soka na mshindi kupatikana kwa haki.
Tunajua kuwa pambano la timu hizo huwa na presha nyingi kuanzia kwa wachezaji, viongozi wa timu, viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na hata wapenzi wa soka, hivyo ni pambano gumu kwa kila upande.
Pamoja na ugumu wote huo hapo ndipo watu wanataka kuona ukomavu wa timu hizo kwa kuweza kuhimili presha hizo pamoja na mambo mengine yote. Kama vile utofauti wa mapato vinapocheza vigogo hivyo na pale zinapocheza timu za kawaida, basi wapenzi wa soka leo wanataka kuona soka la uhakika, ambalo pia litakuwa funzo kwa klabu zingine.
Ni vizuri timu zingine zikajifunza mambo mazuri kutoka kwa vigogo hao badala ya kujifunza mambo mabaya, yakiwemo yale ya kuvunja viti na kuharibu miundo mbinu mingine uwanjani hapo.
Tumeshuhudia uharibufu mkubwa zinapocheza timu hizo mbali na ule wa kuvunja viti, bali hata uhabifu wa koki za mabomba ya maji pamoja na mashabiki wengine na hata kujisaidia haja ndogo katika masinki ya kunawia mikono.
Kuna mambo mengi ya aibu yanayofanyika uwanjani wakati timu hizo mbili zinapocheza na ukiambiwa unaweza usiamini kabisa kama kweli mashabiki wa timu hizo ndio waliofanya vituko hivyo.
Waamuzi nao wamekuwa tatizo kubwa kwani mara nyingi badala ya kuamua mchezo kwa kutumia sheria 17 za soka, wenyewe wamekuwa wakitumia `mapenzi’ yao au ushawishi mwingine.
Ni matarajio yetu kuwa waamuzi wote waliopangwa kuchezesha mchezo wa leo watakuwa fair bila kupembelea upande wowote na hilo litawasaidia kujiansikia historia katika soka la Tanzania.
Na wapenzi wa soka lazima wakubali kuwa mchezo wa mpira wa miguu huwa na matokeo ya aina tatu, yaani kushinda, kushindwa na sare hakuna zaidi ya hapo.
Comments
Post a Comment